Wednesday, April 29, 2009

SIKU 100 ZA RAIS OBAMA IKULU!!

Barack Hussein Obama ametimiza siku 100 leo tangu aapishwe kuwa Rais wa Marekani. Wamarekani wana utaratibu wao wa kijadi wa kupima uwezo wa kiuongozi wa viongozi wao wakianza na siku 100 za kwanza. Ni utaratibu wa kihistoria ambao kwa mujibu wao,huwa unaonyesha dalili za jinsi uongozi wa Rais mpya utakavyokuwa. Misingi,misimamo na hulka ya kiongozi wao huonekana ndani ya siku 100! Obama anazidi kujijengea umaarufu na pia kukijengea chama chake cha Democrat umaarufu.Republican wanazidi kubomoka na kuonekana kushindwa katika nguvu za hoja.

Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali,Barack Obama anazidi kukubalika. Wamarekani wengi wanakiri kwamba anafanya kazi nzuri,ni muwazi na hana zile hulka za kigomvi ambazo marais wengine waliomtangulia walikuwa nazo. Kitendo chake cha kusalimiana na Rais wa Venezuela,Hugo Chavez, hotuba aliyoitoa kule Uturuki,jinsi ambavyo ameanzisha mijadala ya kidiplomasia na nchi kama Iran nk ni baadhi tu ya mifano michache kati ya mingi inayoonyesha Obama ni mtu wa aina gani.Lakini wapo ambao wanasema haeleweki na wala hatabiriki. Bado wafuatiliaji na wakosoaji wa masuala ya kisiasa nchini Marekani wanakuna vichwa vyao kujaribu kumsoma zaidi.

Wakati anaingia madarakani niliwahi kuandika kuhusu tofauti mbalimbali za matarajio ya ulimwengu kwa Obama. Kila mtu alikuwa na bado ana lake.Weusi wengi duniani tunamuona kama kioo au ushahidi kwamba inawezekana na yaliyopita si ndwele bali tugange yajayo.Mashariki ya mbali wanachoomba ni amani.Akiweza kuwaletea amani ya kudumu ni mafanikio ya kutosha.Afrika tunachoomba ni misaada zaidi,kusaidiwa.Tunaamini kwa sababu ni Obama ni “mwanakwetu” basi ni lazima akumbuke alikotoka.

Sasa kama umemfuatilia vizuri Rais Obama utagundua kwamba hajaitamka tamka sana Afrika ndani ya siku 100.Amekuwa akizungumzia zaidi nchi za ulimwengu wa tatu na sio Afrika pekee ingawa nyingi ya nchi hizo zipo barani Afrika.Zaidi aliongelea habari hizi katika mkutano wa G20 huko Uingereza ambapo uwepo wake tu katika mkutano ule ulikuwa ni ishara ya kutosha kwamba huenda yale mabadiliko aliyokuwa anayanadi wakati wa kampeni zake ndio yamewadia. Obama anaonekana kuiangalia dunia kwa mapana zaidi kuliko wengi walivyotarajia.Je hiyo ni kumaanisha kwamba Afrika haipo katika nafasi za juu katika ajenda ya Rais Obama? Sina uhakika.Nampa muda zaidi.Yawezekana ni kutokana na changamoto za hali mbaya ya uchumi wa dunia zinazomkabili. Angalau tunajua hajaacha kumpigia simu “nyanya” ake aliyeko kijijini Kogelo.

Mwisho ni kumpongeza na kumtakia kila la kheri.Akifanya vyema Obama atazidi kuandaa njia ya vizazi vya sasa na vijavyo hususani vya watu weusi.Akichemsha tutaambiwa si mnaona? Tuliwaambia.........

2 comments:

Anonymous said...

miaka mia eh?

Anselm said...

Slip of the finger on the keyboard,siku 100 na si miaka 100.
Bill kama unaweza edit hiyo kitu hapo vinginvyo waoshwa vinywa watapata cha kuongea.